Hosea 11:1-12

Swahili Union Version (SUV)

Mungu anaeleza upendo wake kwa Israeli na Efraimu. Anatoa onyo la adhabu kwa uasi wao.

Swahili Union Version. Bible Society of East Africa.

1Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.

2Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga.

3Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya.

4Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao.

5Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea.

6Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe.

7Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza.

8Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuponya, Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu ? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja.

9Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.

10Watakwenda kumfuata Bwana, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka.

11Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema Bwana.

12Efraimu amenizinga kwa maneno ya uongo, na nyumba ya Israeli kwa udanganyifu; na Yuda hata sasa anasitasita kwa Mungu, na kwake aliye Mtakatifu, naye ni mwaminifu.