Hosea 7:1-16
Swahili Union Version (SUV)
Mungu analaumu Israeli kwa uasi wao. Wanapenda uongo na ubaya.
Swahili Union Version. Bible Society of East Africa.
1Wakati nitakapo kumponya Israeli, ndipo yafunuliwapo maovu ya Efraimu, na ubaya wa Samaria; maana wanatenda uongo, na mwivi huvunja nyumba za watu, na kundi la wanyang'anyi hushambulia nje.
2Wala hawafikiri mioyoni mwao ya kwamba naukumbuka uovu wao wote; sasa matendo yao wenyewe yamewazunguka pande zote; yako mbele za uso wangu.
3Humfurahisha mfalme kwa uovu wao, na wakuu wao kwa uongo wao.
4Hao wote ni wazinzi; wamekuwa kama tanuu iliyotiwa moto na mwokaji; huacha kuuchochea moto, tangu kuukanda unga hata umekwisha kutiwa chachu.
5Sikukuu ya mfalme wetu, wakuu walijitapisha kwa ukali wa divai; alinyosha mkono wake pamoja na wenye mzaha.
6Maana wamefanya moyo wao kuwa tayari kama tanuu, wakati waoteapo; hasira yao hulala usiku kucha; asubuhi yawaka kama moto utoao miali.
7Wote wamepata moto kama tanuu, nao hula makadhi wao; wafalme wao wote wameanguka; hakuna hata mmoja wao aniitaye mimi.
8Efraimu ajichanganya na mataifa; Efraimu ni mkate usiogeuzwa.
9Wageni wamekula nguvu zake, naye hana habari; naam, nywele za mvi zimeonekana huko na huko juu yake, naye hana habari.
10Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; ila hata hivyo hawakumrudia Bwana, Mungu wao, wala hawakumtafuta kwa ajili ya hayo yote.
11Naye Efraimu amekuwa kama njiwa mpumbavu, asiye na fahamu; humwita Misri, huenda Ashuru.
12Watakapokwenda nitatandika wavu wangu juu yao; nitawashusha kama ndege wa angani; nitawarudi, kama vile mkutano wao ulivyosikia.
13Ole wao! Kwa kuwa wamenikimbia; uharibifu na uwapate! Kwa kuwa wameniasi; ingawa ninataka kuwakomboa, hata hivyo wamenena uongo juu yangu.
14Wala hawakunililia kwa moyo, lakini wanalalamika vitandani mwao; hujikutanisha ili kupata nafaka na divai; huniasi mimi.
15Ingawa nimewafundisha na kuwatia nguvu mikono yao, hata hivyo hukusudia udhalimu juu yangu.
16Wao hurudi, lakini si kwake Aliye juu; wamekuwa kama upinde usiotumainika; wakuu wao wataanguka kwa upanga, kwa sababu ya jeuri ya ndimi zao; jambo hili litakuwa kwao sababu ya kuchekwa katika nchi ya Misri.